Kurasa

Jumapili, 20 Julai 2014

VYAKULA NA VINYWAJI KATIKA UIMBAJI




JUZ.1                                                                                               
Julai, 2014.

VYAKULA NA VINYWAJI KATIKA UIMBAJI

Mhuville Humphrey

1.0 Utangulizi
Uimbaji ni taaluma kama zilivyo taaaluma zingine za sheria, elimu, uhandisi, usimamizi wa fedha, biashara na kadhalika. Taaluma hizo na zingine zinautaratibu uliowekwa ili kumfanya mtu asiyejua kujua na hatimaye kuitwa mwanasheria, mwalimu/mwezeshaji, muhandisi au msimamizi wa fedha. Hivyo basi, uimbaji nao una taratibu zake hata mtu akafikia kiwango cha kuthibitika kuwa ni muimbaji ama kwa kupewa cheti au kuonesha uwezo wake mbele ya wengine; kanisani, kwenye majukwaa ya matamasha ya uimbaji na kadhalika.

Kwahiyo, makala hii imelenga kumsaidia muimbaji kumpa sheria na taratibu za uimbaji hususani katika suala zima la chakula gani muimbaji ale au asile na vinywaji gani muimbaji anywe au asinywe ili awe na uwezo wa kuimba vizuri mahali popote.

2.0 Nafasi ya Vyakula na Vinywaji katika uimbaji.
Katika suala la kula na kunywa muimbaji yeyote anaweza kufananishwa na mkimbiaji. Mkimbiaji hawezi kujishindilia chakula kingi au kunywa maji mengi wakati akijua anakwenda kwenye mazoezi au mashindano ya kukimbia umbali wa maili fulani. Hii ni kwa sababu, atashindwa kukimbia vizuri. Hata muimbaji; hawezi kula au kunywa kwa kupitiliza halafu asipate shida wakati wa zoezi la kuimba. Hii ni kwa sababu, kushiba sana kunazuia zoezi la upumuaji wakati wa uimbaji na kusababisha muimbaji kushindwa kutengeneza sauti nzuri za uimbaji. 

Pia, mkimbiaji hatokuwa na nguvu za kukimbia kama hatokula chakula cha kutosha au kunywa maji ya kutosha. Muimbaji halikadhalika, anahitaji kula chakula na kunywa maji kwa kuwa uimbaji ni kazi ngumu ambayo inahitaji virutubisho vya kutia nguvu mwili ambavyo vinapatikana katika vyakula na vinywaji tunavyotumia katika maisha yetu ya kila siku. Hivyo, kula na kunywa ni jambo la muhimu sana kwa muimbaji katika zoezi la uimbaji lakini kwa tahadhali.

2.1 Tahadhali ya vyakula na vinywaji katika uimbaji (nini muimbaji hapaswi kula au kunywa katika siku ya uimbaji na wakati wa uimbaji)
Muimbaji asishinde na njaa au kutokunywa maji kabisa siku ya uimbaji. Hii ni kwa sababu, kutokula kutanyong’onyesha mwili wake hivyo atashindwa kuimba kwa ufanisi. Zingatia: kama muimbaji amefunga; atumie maji (anywe kidogokidogo) ili kulainisha na kulifanya koo lake lisiwe kavu. Pia,  maji yatampa muimbaji nguvu ya kusimama na kuwahudumia watu kwa muda uliopangwa.  

Muimbaji asinywe kinywaji chochote chenye kafeni. Hii hujumuisha vinywaji kama vile; kahawa, cola (soda), chai ya rangi nyeusi (black tea) na vinywaji vyote ambavyo vina cafeni ndani yake. Vinywaji hivi ni kichochezi cha mkojo na hufanya mwili wa muimbaji kushindwa kufyonza maji kunakosababisha mwili kukauka au kuishiwa maji ambayo ni muhimu sana katika kumpa muimbaji nguvu ya kuimba. Pia, vinywaji hivi husababisha; kuzalishwa kwa kitu kama uteute (kamasi) kwenye kinywa na koo, ukavu na maumivu kwenye koo, huleta kiungulia na kusababisha kucheua mara kwa mara wakati wa uimbaji. Zingatia: Kama muimbaji anashindwa kuacha vinywaji hivyo, inashauriwa kusukutua koo kwa maji mara baada ya kunywa kinywaji cha namna hiyo kwa siku nzima ili kusafisha koo na kuepuka athali zisababishwazo na vinywaji hivyo katika uimbaji. Pmoja na hilo, muimbaji anywe maji mengi; zaidi ya glasi nane kwa siku. Au, Muimbaji atumie chai nyeusi (black tea) ambayo inaelezwa kuwa na kiwango kidogo sana cha kafeni. Ila matumizi ya chai ya kienyeji ni bora zaidi (mchaichai).

Muimbaji asile vyakula au kunywa vinywaji vinavyoongeza au kuacha uteute kwenye kinywa na katika koromeo kabla na wakati wa uimbaji. Mfano wa vyakula hivyo ni mayai, maziwa, ‘ice cream’ na bidhaa zingine za maziwa kama pipi, ‘chocolate’, biskuti, keki, siagi, samri, koni na kadhalika. Uteute unaosababishwa na vyakula na vinywaji hivyo huzuia utokaji mzuri wa sauti ya uimbaji wakati wa kuimba. Ndio maana utakuta waimbaji wengine wanahama funguo za muziki au kushindwa kuimba sauti za funguo za juu au kupata tatizo la kushindwa kupanda na kushuka vema kwa sauti wakati wa uimbaji.

Muimbaji asitumie vyakula au vinywaji vinavyokausha koo. Mfano wa vinywaji hivyo ni kama vile; pombe, matunda jamii ya ndimu kama chungwa, limao, chenza, daransi, embe mbichi, na kadhalika. Kukauka kwa koo kutasababisha sauti ya muimbaji kutotoka vema kwasababu koo lake ni kavu.

Muimbaji asitumie soda na vinywaji vyovyote vinavyotoa povu wakati vinapofunguliwa. Vinywaji hivi huweka gesi/hewa tumboni na kumfanya muimbaji kubeu na/au kucheua hovyo na kusababisha muimbaji kupata shida wakati wa kuimba na kutoa sauti mbaya. 

Muimbaji asile vyakula ambavyo vitaacha vitu kama makapi kwenye koo lake. Vyakula hivyo ni kama vile; bisi, mahindi, karanga, tambi kavu, chama, na kadhalika. Ulaji wa vyakula hivi kabla na wakati wa kuimba husababisha ugumu wa utoaji wa sauti za kuimbwa. Pia, makapi hayo wakati mwingine hurukia katika koo la chakula na kusababisha muimbaji kupaliwa na hatimae muimbaji kushindwa kupumua vema, kukohoa na kuimba vibaya. 

Muimbaji asile vyakula vya mafuta sana kama vile nyama zilizonona na kadhalika. Pia, sukari nyingi haifai kwa muimbaji. 

Muimbaji asile vyakula au vinywaji vinavyoleta mwasho au kukera koo (throat irritants), vinavyochangamsha, kusisimua au kulewesha (Overly spicy foods) kama vile; kahawa na pilipili, vinywaji baridi sana, sukari iliyosafishwa, chocolate na kadhalika.

Muimbaji asitumie Jamii ya vitu vyenye alkoholi, Sigara, tumbako, bangi, ugoro na aina yoyote ya madawa ya kulevya kwakuwa vinaathali kubwa kwenye koo na mapafu ambavyo ni viungo muhimu sana katika utengenezaji wa sauti bora za uimbaji.

Muimbaji asitumie vyakula vyenye madhara kwa mwili wake (mzio; allege). Kwa mfano, baadhi ya waimbaji hupata shida baada ya kula matunda jamii ya machungwa, ngano, karanga, samakigamba, soya na kadhalika.
Muimbaji asitumie vyakula vyenye mafuta mengi, na nyama nyekundu kama ya ng’ombe, mbuzi na kadhalika.

2.2 Vyakula na vinywaji vitakavyofanya muimbaji aimbe vizuri (vyakula na vinywaji ambavyo muimbaji anashauriwa kuvitumia kabla na /au wakati wa uimbaji)
Muimbaji ale chakula cha wastani (kiwango cha kutosheka) masaa mawili kabla ya uimbaji. Hii itasaidia chakula kumengenywa vema na kumpatia muimbaji nguvu wakati wa kuimba. Kushiba sana (kuvimbiwa) husababisha tumbo kushindwa kumeng’enya chakula kwa haraka na hivyo kutamfanya muimbaji ashindwe kutoa sauti vema. Hii ni kwa sababu, tumbo litashindwa kusukuma hewa kutoka nje ili kutengeneza sauti nzuri za uimbaji. Pia, muimbaji atakuwa anabeua na kucheua hovyo wakati wa kuimba hali ambayo humfanya kutoa sauti mbaya au kushindwa kuimba kabisa.

Muimbaji anywe maji ya kawaida (room temperature water) yaani yasiwe ya moto wala ya baridi au barafu. Maji hayo yanywewe masaa mawili kabla ya uimbaji. Maji haya yatampa nguvu muimbaji, yatafanya koo la muimbaji kuwa bichi (sio kavu) na mwili kutokuwa mkavu. Muimbaji hanabudi kutambua kuwa matumizi ya maji ya moto hutanua na maji ya baridi (au barafu) husinyaza/hubana koromeo hivyo kusababisha kiboksi cha sauti kushindwa kutengeneza sauti za kuimba vizuri na muimbaji ataimba vibaya. Zingatia: Unaweza kunywa maji ya moto au ya baridi baada ya uimbaji na sio kabla au wakati wa uimbaji. 

Muimbaji ale matunda yenye maji mengi kwa ajiri ya kuufanya mwili wake kufyonza maji na kupata nguvu. Mfano wa matunda hayo ni pamoja na tikiti maji, tango na kadhalika.

Muimbaji ale mboga za majani zenye maji mengi kwa ajiri ya kuufanya mwili kupata maji, chumvichumvi na madini ambavyo vyote ni virutubisho vitakavyompa muimbaji nguvu ya kuimba na kutoa sauti yake vizuri wakati wa kuimba. Mfano wa mboga hizo ni pamoja na mchicha, tembele, ‘spinach’, ‘chinise’, na kadhalika.
Muimbaji anaweza kutumia asali, na chumvi kidogo ni nzuri kwa koo la lake katika siku ya uimbaji.

Matumizi ya chai ya mitishamba (mchaichai) ni bora zaidi kwa afya ya koo na tumbo lako ili kusaidia utengenezaji wa sauti nzuri za uimbaji.

3.0 Hitimisho na mapendekezo.
Koo hupendezwa, hutulizwa, huburudishwa, hutengenezwa na aina fulani ya pipi, asali, mvuke, chai ya mitishamba (mchaichai), kusafisha koo kwa maji chumvi, baadhi ya dawa kwa ushauri wa daktari, unywaji wa maji, na kadhalika. Pia, kinyume chake koo laweza kuharibiwa na matumizi ya vyakula au vinywaji kama vile; pombe, kahawa, soda, maziwa, chokoleti, pipi, ubuyu, matunda jamii ya ndimu, mayai, karanga, mahindi, bisi na kadhalika. Hivyo, muimbaji awe na taadhali katika matumizi ya vyakula na vinywaji ili kufanya sauti yake kuwa bora na kupendeza mbele za watu na Mungu tunayemtukuza kupitia sauti zetu.

Mathalani, mwanafunzi mzuri ni yule anayetafuta zaidi maarifa mara baada ya kujifunza jambo fulani. Hivyo, ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya yatakuwa msingi bora kwa muimbaji kutafuta zaidi kwa habari ya vyakula na vinywaji katika uimbaji. Haya yalioelezwa hapa ni machache sana.

Pamoja na hayo, mabadiliko chanya ya uimbaji yatategemea uzingativu na utekelezaji kwa vitendo wa mambo hayo na sio kusikiliza tu. Pia, mabadiliko hasi yatatokea kwa wasiozingatia na kutekeleza kwa vitendo mambo hayo. Yuko mshairi anasema,
“Mshumaa tuliwasha, ili nuru kumulika,
Giza kulitokomesha, na nuru kuenezeka,
Mshumaa unawaka, giza mbona linazidi?”

Pia, mshairi mwingine anasema,
“Mnazi walioukwea,
Shinani wameanzia,
Si kama mejirukia,
Kileleni taka tua,
Jikazie yako kwego, mnazi upate kwea.”
Hivyo, huu ni mwanzo wa kujifunza uimbaji; huna budi kuifuata nuru (mafunzo) unayoangaziwa (kupewa) ili ufanikiwe katika uimbaji. Hii ni kwa sababu, wote waliofanikiwa katika aina yoyote ile ya huduma, walianzia chini na kwa kuwa walisikiliza na kutekeleza waliyoelekezwa na viongozi wao wakaweza kupanda na leo hii ni watu wakuu katia huduma.

Mithali 4:10, 13, 18, 19, 20, 21, na 22 inasema,
“10 Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa   mingi…
13 Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako…
18 Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu.
 19 Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho.
 20 Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu.
 21 Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako.
 22 Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote.”
Hivyo, ni vema kuyafuata, kuyazingatia na kuyatendea kazi maarifa yote uliyopewa ili ufanikiwe kiuimbaji kwani asiyefuata hayo anafananishwa na kama vile inavyofafanuliwa na mwandishi wa Mithali 1:7b; anasema,
“Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.”










Mhuville Humphrey, Mwl. Kiongozi - Kusifu na Kuabudu ECWC-Mji wa Bwana Mbezi
0652 516 581/0685736581
BAed-St. John’s University of Tanzania 2011/2014

Maoni 16 :

  1. As ante sana nimekuelewa je na Maji ya vuguvugu nayo yanafaaa?

    JibuFuta
    Majibu
    1. Mazoezi pia Ni ya muhimu ktk uimbaji kutegeneza pumuzi ya kutosha

      Futa
    2. Maji yeyote tu kwasababu kinachohitajika ni unyevu kooni yani ya viguvugu au yasiyovuguvugu.

      Futa
    3. Maji yeyote tu kwasababu kinachohitajika ni unyevu kooni yani ya viguvugu au yasiyovuguvugu.

      Futa
    4. Maji yeyote tu kwasababu kinachohitajika ni unyevu kooni yani ya viguvugu au yasiyovuguvugu.

      Futa
  2. Nimepata fundisho mm Kama muimbaji katika swala la kunywa na kula vyakula ambavyo vitamfanya mtu aimbe vizuri

    JibuFuta
  3. Na vipi kuhusu mayai mabichii hii miekaaje?

    JibuFuta
  4. Vp kuhusu mayai kama alivyo uliza ndg hapo juu
    "je, yanatumiwaje ?"

    JibuFuta
  5. Ahsante sana ila nimetiya swali hapo juu👆👆👆

    JibuFuta
  6. Ahsante sana ila nimetiya swali hapo juu👆👆👆

    JibuFuta
  7. Vp kuhusu mayai kama alivyo uliza ndg hapo juu
    "je, yanatumiwaje ?"

    JibuFuta
  8. Swali lingine ni : "Vp kuhusu maji ya moto na asali kwa pamoja ?"

    JibuFuta
  9. Vp kuhusu kunywa vinywaj vya baridi kupi
    ta kias je hilo haliwez kuwa tatizo kwa muimbaj

    JibuFuta
  10. Naomba kuuliza nizoezi gani lakuifanya sauti yangu ijae au iwe nauzito

    JibuFuta
  11. Imekaa vizuri elimu iongezwe zaidi ili tutambue jinsi ya kuweza kupafom vizuri hilo la mayai tupeni mawlekezo mliotutangulia ktk huduma hii jamen

    JibuFuta